Sunday 24 June 2007

Watumishi wasiofuata maadili washughulikiwe - JK

007-06-24 09:57:17
Na Raymond Kaminyoge

Rais Jakaya Kikwete ameagiza watendaji wakuu, kuwashughulikia haraka watumishi wasiofuata maadili katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Rais Kikwete alisema hayo jana, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika kilele cha wiki ya utumishi.

Alisema watumishi wa umma wanalo jukumu la kuwapa huduma bora wananchi kwa kufuata maadili bila kuwabagua.

Alisema serikali itaendelea kupambana na uzembe kwa nguvu zake zote hadi utumishi wa umma utakapokuwa safi na uliotukuka.

Alisema utumishi wa umma umeshajiwekea kanuni na maadili ya kiutendaji ambayo watumishi wanayajua na kilichobakia ni kuyatekeleza kwa dhati katika kuwahudumia wananchi.

Alisema kuwashughulikia watumishi ambao hawafuati maadili kunahitaji viongozi wenye tabia ya kutowaonea aibu watumishi wasioyafuata.

Alisema watumishi wa umma wanatakiwa kubadilika kwa kutoa huduma bora kwa wananchi wakati serikali inaendelea kuboresha maslahi yao.

``Wakati serikali inaboresha maslahi na mazingira ya kufanyia kazi, watumishi warudishe fadhila hizi kwa kuwahudumia wananchi ambao wanatoa kodi ambazo zinawawezesha wao kulipwa mishahara`` alisema.

Aidha, aliwataka kuwa mstari wa mbele katika kupambana na rushwa ikizingatiwa kuwa utumishi wa umma ndiyo injini ya serikali katika kutekeleza majukumu yake.

``Kama mtumishi atagubikwa na rushwa, basi hali hii itaenea hata katika sekta nyingine binafsi ambazo zinautegemea utumishi wa umma kufanikisha kazi zake,`` alisema.

Rais Kikwete alisema kipimo cha mafanikio katika utumishi ni kupata majibu chanya katika masuala ya msingi yanayopima utekelezaji wa maboresho ya utumishi wa umma.

``Mnatakiwa kujiuliza, wananchi leo wanaheshimiwa na kuhudumiwa vizuri kuliko ilivyokuwa awali, au je, ni kwa kiasi gani watumishi wa umma wanazingatia maadili ya kazi zao na taaluma,``alisema.

Rais Kikwete aliongeza kuwa ni lazima utumishi wa umma uwe na mfumo wa mrejesho katika utoaji wa huduma toka kwa wananchi.

Alisema mrejesho huo utumiwe na asasi mbalimbali za serikali ili hatimaye utumike kufanya marekebisho katika maeneo ambayo huduma hazijaboreshwa.

``Lakini cha msingi zaidi tuwe na utaratibu na utamaduni wa kuwasikiliza wananchi, hili litachangia sana kwenye kupambana na watumishi wasio waadilifu, kupambana na rushwa na kutatua kero za wananchi,`` alisema.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi Hawa Ghasia alisema wiki ya utumishi wa umma imeenda sambamba na maonyesho ya taasisi za serikali.

Alisema jumla ya taasisi 77 zimeshiriki katika maonyesho ya mwaka huu ikilinganishwa na taasisi 27 ambazo zilishiriki mwaka jana.

``Kupitia maonyesho hayo kero nyingi zimeweza kutambuliwa kutoka kwa wadau ambazo ama tumezifanyia kazi au tunaendelea kutafuta majawabu kwa lengo la kuboresha huduma tunazozitoa kwa umma.

Alisema katika maonyesho yaliyopita, wadau wengi walilalamika kuwa kwa muda mrefu hawakuwa wamepandishwa vyeo.

Alisema baada ya malalamiko hao, ofisi yake ilishughulikia kero hizo na kupunguza tatizo hilo kwa asilimia kubwa.

Alisema ili kuboresha maadhimisho hayo na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kufaidika na huduma za umma, miaka ijayo wizara hiyo itafanya maonyesho hayo kwa zamu katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Rais Kikwete aliwakabidhi washindi tuzo za utoaji wa huduma bora ambazo mshindi wa kwanza ni Wakala wa Mkemia wa Serikali, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na wizara ya Fedha ambayo ndiyo mshindi wa tatu.

* SOURCE: Nipashe

No comments: