Sunday 29 July 2007

Ukaguzi wa magari nje wachefua wabunge

Ukaguzi wa magari nje wachefua wabunge
Halima Mlacha, Dodoma
HabariLeo; Saturday,July 28, 2007 @00:03
WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa upinzani, jana walimtaka Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Basil Mramba, kufuta uamuzi wa kuteua mawakala maalumu wa kukagua magari nje ya nchi yanayoingia nchini.

Chini ya utaratibu huo, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limeteua mawakala maalumu wa kukagua magari nje ya nchi yanayoingia nchini.

Kwa sasa, tayari ipo sheria ya Kudhibiti Uingizwaji wa Magari Chakavu na Mamlaka ya Mapato (TRA), ndio wanaofanya ukaguzi huo na mwenye gari hulazimika kulipia ushuru zaidi kama gari lake ni la zaidi ya miaka 10.

Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara, Abdallah Sumry (CCM), alisema kamati inaiona tenda hiyo ya ukaguzi wa magari nje, kama ni usumbufu kwa Watanzania na njia ya baadhi ya watu kujipatia kipato cha bure.

“Kamati inaona ukaguzi huu wa magari nje ya nchi yanayoingia Tanzania ni usumbufu kwa Watanzania na ni aina fulani ya watu kujipatia kipato bure tena cha fedha za kigeni kisichofaidisha nchi,” alisema mbunge huyo wa Mpanda Magharibi (CCM).

Alisema kwa sasa tayari ipo sheria ya Kudhibiti Uingizwaji wa Magari Chakavu na Mamlaka ya Mapato (TRA), ndio wanaofanya ukaguzi huo na mwenye gari hulazimika kulipia ushuru zaidi kama gari lake ni la zaidi ya miaka 10.

Alisema kamati hiyo inashauri ukaguzi huo usiendelee ili kutowabebesha mizigo mizito Watanzania wanaoagiza magari kutoka nje na kusisitiza juu ya umuhimu wa sheria hiyo iliyopitishwa bungeni kufanya kazi yake kama ilivyokusudiwa.


Naye Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Lucy Owenya Viti Maalumu (Chadema), alisema mpango huo wa kuteua mawakala kutoka nchi za nje kwa ajili ya ukaguzi wa magari yanayoingia nchini, umepitwa na wakati.

Alisema hiyo ni kutokana na hatua ya Wizara ya Fedha kupitisha Sheria ndogo kwamba magari yenye umri zaidi ya miaka 10 lazima yatozwe ushuru mkubwa. “Kwa maana hiyo hakuna mtu atakayeingiza gari mbovu kutokana na kipengele hicho,” alisisitiza Owenya.

Alisema kambi hiyo inaona kuwa kitendo hicho ni njia ya kuwatafutia baadhi ya watu ulaji kwa jasho la Watanzania wanaoleta magari nchini, na alizitaja baadhi ya nchi ambazo TBS imewateua wakala wa kukagua magari hayo kuwa ni Dubai, Hong Kong, Thailand, Japan na Uingereza.

Naye Mbunge wa Solwa, Ahmed Ally Salum (CCM), alisema anasikitishwa na utaratibu huo ulioanzishwa kwani umewafaidisha wachache na kuwakandamiza zaidi Watanzania wanaojitahidi kujikwamua na umasikini.


“Hivi wakati gari inapigwa ushuru chakavu wewe unalikagua tena la nini, tunaomba Waziri Mramba uondoe tatizo hili kwani linamnufaisha tu aliyekuwa akiongoza mradi huu ambaye kwa sasa inasemekana amejenga nyumba yenye thamani ya dola za Marekani milioni 600,” alisema Salum.

Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), akichangia makadirio ya wizara hiyo, aliwataka Watanzania kubadilika na kuacha kununua malighafi kutoka nje ya nchi na badala yake watumie za ndani.

Alitolea mfano viti na kapeti la Bunge pamoja na suti za watu wengi waliovaa, kuwa ni malighafi kutoka nje hali inayochangia Shilingi ya Tanzania kushuka. “Wakoloni zamani walikuwa wakitumia malighafi za hapa kwetu na kutengeneza makochi, meza, lakini sasa hivi tunapenda vitu vya nje mpaka dawa ya mswaki,” alisema.

Naye Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Chadema), aliiomba serikali ianzishe mkakati wa kuinua wafanyabiashara tangu ngazi za chini kwa kuanzia na wafanyabiashara wadogo (wamachinga).

“Tusiache wale wafanyabiashara haramu kama vile wauza dawa za kulevya ndio baadaye waje waibuke kuwa wafanyabiashara wakubwa, lazima tujenge wafanyabiashara watakaojenga nchi hasa hawa wamachinga,” alisema Ndesamburo.

Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Basil Mramba, akiwasilisha makadirio na matumizi ya fedha ya wizara yake, alisema katika kuimarisha viwanda na biashara nchini, wizara hiyo ina mpango wa kuanzisha miji au vitovu vya biashara pamoja na kuanzisha kituo cha kwanza cha kimataifa cha biashara kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji.

Hata hivyo, Mramba alizitaka taasisi za fedha zenye kutoa masharti magumu kuacha tabia hiyo kwa kisingizio cha walengwa kutokopesheka badala yake zianze kutoa mikopo ili kuinua sekta ya viwanda na biashara nchini.


Pamoja na hayo aliwataka wananchi kuendeleza ujasiriamali na uzalendo kwa kutoa kipaumbele katika ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa nchini ikiwa ni pamoja na serikali na taasisi kutoa zabuni kwa wazalendo.


Alisema sekta hiyo ya viwanda kwa sasa ina mafanikio makubwa kwani uchangiaji wake katika pato la taifa umeongezeka kutoka Sh bilioni 200.8 mwaka 2005 hadi Sh bilioni 218.1 mwaka jana.

No comments: